,

,

,

,
Sports

YANGA WAOMBA KUHAMIA ZANZIBAR BAADA YA TAIFA KUFUNGIWA

YANGA SC imeomba kutumia Uwanja wa Amaan, Zanzibar kwa mechi zake mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Taarifa ya Kaimu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit imesema kwamba hatua hiyo inafuatia Serikali kuizuia klabu hiyo pamoja na mahasimu wao, Simba SC kutumia Uwanja wa Taifa.
Yanga imeiandikia barua Wizara ya Habari Utakii na Michezo Zanzibar kuomba kuhamia Uwanja wa Amaan, baada ya kufungiwa kwa Uwanja wa Taifa.

Juzi, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye alitangaza kuzuia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya vurugu zilizosababisha uharibifu Jumamosi katika mechi baina ya watani hao wa jadi.
Mashabiki wa Simba Jumamosi walifanya vurugu Uwanja wa Taifa baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
Nape alisema kwamba mbali na uvunjwaji wa viti, pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na lingine wa Simba yamevunjwa.
Awali ya hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Nkenyenge alisema kwamba zaidi ya viti 1781 vilivunjwa juzi katika mchezo ambao kati ya Sh. Milioni 350 na 400 zikikusanywa katika viingilio vya mashabiki waliingia kwa tiketi za Elektroniki

Jozey The Boy inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Instagram na Twitter ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment

copyright © 2016 Jozey The Boy. Powered by Blogger.