Bodi
ya Wadhamini ya chama cha Wananchi (CUF) imefanya kikao chake Oktoba 2,
2016 katika Makao Makuu ya Chama hicho mjini Zanzibar chini ya
Mwenyekiti wake, Abdallah Said Khatau ili kujadili wito wa Profesa
Ibrahim Lipumba wa kukutana leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kujadili msimamo na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.
Baada ya kikao hicho kufanyika, jana bodi hiyo imetoa tamko lake juu wa wito huo.
Wakati akisoma tamko hilo, Khatau alisema wajumbe wa bodi ya wadhamini wameupuuza wito wa Lipumba.
“Bodi
imepuuza wito wa mtu anayeitwa Lipumba alioutangaza juzi kwamba eti
amemtaka mtu mwengine anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao cha Bodi ya
Wadhamini. Lipumba kwa sasa si Mwenyekiti tena wa CUF na pia si
mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi
la Taifa,” alisema.
Khatau
alisema bodi hiyo itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa la CUF kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5), ambalo ndilo
linaloiteua bodi na kwamba litaheshimu maamuzi yake yote kwa kuwa ndiyo
chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa CUF.
Licha ya kugoma kuitikia wito huo wa Lipumba, Khatau alisema bodi
Itachukua
hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na
98(4) ya katiba ya CUF kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za
Chama alizodai zilivamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Lipumba na genge lake
ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam.
“Pia
itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya
98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka alipe gharama na hasara zote
alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama,
tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza na
genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na
hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban
Sh. 600 milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es
Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban
Sh. 50 milioni,” alisema.
Aidha,
alisema bodi ya wadhamini inawahakikishia wanachama wote wa CUF wa
Tanzania Bara na Zanzibar kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na
itasimama pamoja nao kulinda mali zote za Chama hicho.
0 comments:
Post a Comment