Baraza la Mawaziri nchini Burundi,
kwa kauli moja limeidhinisha mswada wa kuliondoa taifa hilo kutoka kwa
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.
Serikali ya nchi hiyo tayari imewasilisha mswada huo bungeni ambapo unatarajiwa kujadiliwa na hatimaye kuidhinishwa.Makamu wa rais Gaston Sindimwo amesema serikali ya Burundi haiogopi kutengwa zaidi na jamii ya kimataifa.
"Wajua, huenda tukatengwa. Lakini ni sawa mradi tu tuwe tunajivunia uhuru wetu. Ni nchi ngapi hazijajiunga na mahakama hii? Zimetengwa? Kuna Marekani, Urusi, Uchina na nyingine nyingi na kun ahata mataifa jirani hapa ambayo hayajajiunga na mahakama hiyo," alisema.
"Lakini bado yameendelea kuwepo. Hatufanyi chochote kibaya. Ni haki yetu kujitoa mahakama ya ICC. Ni uamuzi wetu; mswada sasa umewasilishwa bungeni. Tuko tayari kwa matokeo yoyote."
Zaidi ya watu 400 wameuawa kwenye machafuko yaliyotokea tangu rais Pierre Nkurunziza aamue kuwania urais kwa muhula wa tatu Aprili mwaka wa 2015. Wengine 200,000 wametorokea mataifa jirani wakihofia usalama wao.
Wafuasi wa serikali na wale wa upinzani pia wamekuwa wakiuawa mara kwa mara katika mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Pierre Nkurunziza ni nani?
- Alizaliwa 1964
- Alikuwa kiongozi wa waasi lakini baadaye akawa rais
- Ni Mkristo
- Alikuwa mwalimu wa michezo
- Hupenda sana kuendesha baiskeli na kucheza kandanda
- Ameoa na ana watoto watano
- Babake aliuawa wakati wa vita vya kikabila mwaka 1972
0 comments:
Post a Comment