Kuelekea uchumi wa viwanda nchini, serikali imefanikiwa kufufua na kuanzisha viwanda ambapo kwa sasa vinavyofanya kazi vipo zaidi ya 52,000. Sekta hiyo pia imetajwa kuwa inatarajia kukuza uchumi wa watanzania asilimia 40.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya viwanda Tanzania yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam kuanzia Disemba 7 hadi 1, 2016.
“Kuelekea ujenzi wa uchumi wa viwanda, nilipewa maelekezo kufanya mambo matatu, ikiwemo uhakikisha vilivyopo ambavyo vingi vilikuwa vinazalisha chini ya kiwango vinaongeza uzalishaji, pili vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi vinafanya kazi na la mwisho nilipewa agizo la kuhakikisha wekezaji wa ndani na nje ya wanakuja kuwekeza,” amesema na kuongeza.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu serikali hii iingie madarakani, kuna viwanda 52,000 vinafanya kazi na kwamba asilimia 40 ya watanzania uchumi wao utatokana na viwanda.”
Aidha, Mwijage amesema Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia taasisi yake ya Mamlaka na Maendeleo ya Biashara Tanzania, imeandaa maonesho yatakayokutanisha wadau wa sekta ya viwanda kwa lengo la kutangaza pamoja na kujadili fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema maonesho hayo pia yatatoa taswira ya juhudi za ujenzi wa viwanda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.